Pages

DK.SLAA AMPIGA CHENGA JK MSIBANI(GAZETI MWANANCHI)


AKWEPA KUKAA JUKWAA KUU, WENGI WAMZIKA REGIA
Juma Mtanda na Shakila Nyerere, Ifakara
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willbrod Slaa, jana alimkwepa tena Rais Jakaya Kikwete safari hii ikiwa katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya chama hicho, Regia Mtema yaliyofanyika katika Kijiji cha Lipangalala.Tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010, ambao Dk Slaa alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 2,271,941 sawa na asilimia  26.34 akiwa nyuma ya Rais Kikwete aliyepata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17, Dk Slaa hakuwahi kukutana na mkuu huyo wa nchi ana kwa ana.
Katika hafla ya kutangazwa matokeo ya urais iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, Dk Slaa hakuhudhuria tofauti na ilivyokuwa kwa waliokuwa wagombea wenzake wote.
Jana, Dk Slaa tofauti na viongozi wenzake wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, hakutaka kujiweka katika mazingira ambayo yangemkutanisha na Rais Kikwete katika mazishi hayo.
Nyumba kulikofanyika shughuli za awali za mazishi, waandalizi waliandaa majukwaa mawili, moja maalum kwa ajili ya wabunge huku jingine likiwa ni maalumu kwa ajili ya viongozi wakuu ambalo alikaa Mbowe, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe.
Mbali ya kukaa viongozi hao, kulikuwa na nafasi ambayo ilikuwa imetengwa maalumu kwa ajili ya Rais. Mbali ya nafasi hiyo, pia kulikuwa na kiti ambacho ilitegemewa kwamba Dk Slaa angekalia.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo wa Chadema alikikwepa na kwenda kujichanganya katika jukwaa la wabunge na kiti hicho kubaki bila ya kuwa na mtu.
Hata hivyo, Rais Kikwete hakuweza kufika nyumbani hadi mwili wa marehemu Regia ulipopelekwa katika Viwanya vya Viungani ambako uliagwa na mamia ya waombolezaji.
Uwanjani hapo nako kulikuwa na majukwaa mawili. Kama ilivyokuwa nyumbani, jukwaa moja lilikuwa la wabunge na jingine la viongozi wa ngazi za juu lakini bado, Dk Slaa alilikwepa jukwaa hilo ambalo Rais alitarajiwa kuwa angefikia. Rais hakuweza kufika Viungani pia.
Rais Jakaya Kikwete akiweka udongo kwenye kaburi la aliyekuwa mbunge wa viti maalum (Chadema) Regia Mtema wakati wa mazishi yaliyofanyika kwenye makaburi ya Ipangalala Ifakara mkoani Morogoro jana.Picha na Juma Mtanda
Baadaye wakiwa eneo la mazishi, Rais Kikwete alifika na kushiriki tukio hilo na kisha kusalimiana na wabunge mbalimbali na viongozi waliokuwa wamefika akiwemo Mbowe, Mbunge wa Rombo Joseph Selasini, Zitto na viongozi wengine lakini Dk Slaa hakuonekana.
Ilitegemewa kuwa tukio hilo la msiba lingewaleta wanasiasa hao lakini hadi Rais Kikwete alipoondoka hakuna mahali ambako walisalimiana.
Mbali ya tukio hilo, hata katika hafla mbalimbali ambazo viongozi wa Chadema wamekuwa wakialikwa ikiwemo Ikulu, Dk Slaa hakuwahi kuhudhuria.
Novemba mwaka jana viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe, walifanya mazungumzo na Rais Kikwete, Ikulu ya Dar es Salaam kujadili suala la Katiba Mpya, lakini Dk Slaa hakuhudhuria.
Chadema wahaha
Wakati viongozi wa Chadema wakihaha kumaliza mgogoro ndani ya chama hicho wilayani Kilombero, Pacha wa marehemu Regia, Remigia Mtema amesema ndugu yake Regia alikuwa akipeleka malalamiko kwa Dk Slaa mara kadhaa kuomba asuluhishe bila mafanikio.
Hata hivyo, Remigia alisema marehemu Regia alikuwa amepanga kuonana tena na Dk Slaa katika siku za hivi karibuni kumweleza kinachoendelea.
Akizungumzia suala hilo, Dk Slaa alisema alishaanza kushughulikia mgogoro huo lakini msiba huo ndiyo uliomkwamisha.
“Ni kweli nimekuwa nikielezwa tatizo hilo na tayari nilishaanza kulifanyika kazi ila sasa siwezi kusema suala hilo limefikia wapi kwani wote tuko kwenye mazishi,” alisema.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wabunge wa Chadema waliotangulia kufika katika msiba huo, Mchungaji Peter Msigwa, Ezekia Wenje na Lucy Owenya, walikutana na uongozi wa kata wa Chadema ili kumaliza mgogoro huo.
Katibu mwenezi wa Chadema kata ya Ifakara, Antony Kamonalelo alisema viongozi hao walikaa na wanachama hao na kuwataka wapunguze munkari ili kumruhusu Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kilombero, Salum Ngozi na Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Kiwanga kuhudhuria mazishi.
Hata hivyo, inadaiwa kwamba wanachama hao waliukubalia uongozi huo kumruhusu Susan peke yake kuhudhuria mazishi hayo.
Juzi, wanachama hao walimtimua msibani Ngozi kiasi cha kuwalazimu polisi waliokuwa eneo hilo kuingilia kati kwa kumchukua mwenyekiti huyo na kumpeleka katika Kituo cha Polisi Wilaya.
Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Ngozi kutimuliwa katika msiba huo. Mara ya kwanza ilikuwa siku moja iliyotangulia ambayo ilimlazimu Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Francis Miti kuingilia kati.
Ngozi amekuwa akidai kwamba anafanyiwa fujo na kikundi cha watu aliowaita wahuni na kwamba amefungua kesi ya kufanyiwa vurugu katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Kilombero na kwamba baada ya kumalizika kwa mazishi.www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment